Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zaahidi kuondokana na ukatili dhidi ya watoto ikiwemo adhabu ya viboko

Mizozo na ukosefu wa utulivu vinaweza kuchochea viwango vya juu vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, wanawake na wasichana
© UNICEF/STARS/Kristian Buus
Mizozo na ukosefu wa utulivu vinaweza kuchochea viwango vya juu vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, wanawake na wasichana

Nchi zaahidi kuondokana na ukatili dhidi ya watoto ikiwemo adhabu ya viboko

Haki za binadamu

Uganda na Burundi ni miongoni mwa nchi zaidi ya 100 duniani zilizochukua hatua ya kihistoria kuahidi kumaliza ukatili dhidi ya watoto, ikiwemo kupiga marufuku adhabu ya viboko, suala linaloathiri watoto 3 kati ya 5 majumbani mwao. Ahadi hizi zimetolewa katika mkutano muhimu uliofanyika Bogotá, Colombia, unaolenga kukubaliana juu ya tamko jipya la kimataifa la kuwalinda watoto dhidi ya aina zote za ukatili, unyonyaji, na dhuluma.

Taarifa iliyotolewa nashirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO huko Bogota, Colombia hii leo, inasema Uganda, Burundi na Gambia, zimeahidi kufuatilia sheria dhidi ya adhabu ya viboko katika mazingira yote huku Nigeria ikisema itafuatilia kuondokana na adhabu  hiyo shuleni.

Mkutano huu, ulioandaliwa kwa pamoja na serikali za Colombia na Sweden, Shirika la Umoja wa Mataifa lile la la Afya Ulimwenguni (WHO), na lile la Kuhudumia watoto (UNICEF), na Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto, ulishuhudia nchi kadhaa zikiahidi kuboresha huduma kwa waathirika wa ukatili wa watoto na kuwekeza katika msaada wa malezi. 

Harakati ni kutokomeza ukatili majumbani na shuleni

Hatua hizi zinachukuliwa ili kupunguza hatari za ukatili majumbani, huku baadhi ya nchi zikiahidi kukabiliana na udhalilishaji shuleni na kuanzisha mipango ya usalama wa kidijitali.

“Ukatili dhidi ya watoto ni changamoto kubwa inayoweza kuzuilika, lakini bado ni ukweli wa kila siku kwa mamilioni ya watoto duniani kote, ukiacha makovu ya kudumu,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Kwa mujibu wa takwimu za WHO, zaidi ya nusu ya watoto ulimwenguni, takribani bilioni moja, wanakabiliwa na aina fulani ya ukatili. Ukatili huu ni pamoja na unyanyasaji wa kimwili, kihisia, na dhuluma za kingono. Ripoti zinaonesha kuwa chini ya asilimia 10 ya watoto waliokumbwa na ukatili hupata msaada wowote, hali inayozua hofu kuhusu hatma ya vizazi vijavyo.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa ukatili dhidi ya watoto huongeza hatari ya matatizo ya muda mrefu ya kiafya na kiakili. 

Madhara ya ukatili dhidi ya watoto ni pamoja na kifo

Kwa baadhi ya watoto, husababisha kifo au majeraha makubwa, huku wengine wakipata athari za kudumu kama wasiwasi, unyogovu, na tabia hatarishi. Kila dakika 13, mtoto au kijana mmoja hufariki kutokana na mauaji – ikikadiriwa kwamba karibu vifo 40,000 vinaweza kuepukika kila mwaka.

WHO inasisitiza kuwa ukatili huu unaweza kuzuilika kwa kutumia mikakati thabiti kama elimu ya malezi kwa wazazi ili kujenga uhusiano chanya na watoto wao, mipango ya shuleni kuzuia unyanyasaji, sheria kali dhidi ya ukatili kwa watoto, na kuhakikisha usalama wa watoto mtandaoni.

 Utafiti unaonesha kuwa nchi zikitekeleza mikakati hii kikamilifu, zinaweza kupunguza ukatili kwa watoto kwa kiwango cha asilimia 20-50.

Zaidi ya watu 1,000 wanahudhuria mkutano huu wa kwanza wa mawaziri kuhusu ukatili dhidi ya watoto, ukiwaleta pamoja viongozi wa serikali, watoto, na wadau wa kiraia. Ahadi mbalimbali zimetolewa, zikiwemo kuanzisha programu za usalama mtandaoni, kuongeza umri wa ndoa kisheria, na kuwekeza katika elimu ya malezi.

 WHO inaahidi kuendelea kushirikiana na nchi zote katika juhudi hizi za kukomesha ukatili dhidi ya watoto.