Sasa maandamano na kujieleza kwa uhuru ni ruhusa Bangladesh - Yunus
Sasa maandamano na kujieleza kwa uhuru ni ruhusa Bangladesh - Yunus
Mshauri Mkuu wa serikali ya mpito nchini Bangladesh, Muhammad Yunus amehutubia Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA79 jijini New York, Marekani na kueleza mambo ya msingi wanayofanya hivi sasa ili kurejesha utawala wa haki na wa amani nchini humo baada ya maandamano yaliyosababisha Waziri Mkuu kukimbia nchi.
Akihutubia kwa lugha ya kibangla na kutafsiriwa kwa lugha zote 6 rasmi za Umoja wa Mataifa, Bwana Yunus ametaja mambo hayo kuwa ni pamoja na uhuru wa wananchi kukusanyika na kutoa maoni yao bila vikwazo, uhuru wa vyama vya siasa kueleza hoja zao bila kubinywa, uhuru wa mahakama na pia uhuru wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.
Vile vile amesema kwa viongozi wa umma, wamewekewa utaratibu wa kuhakikisha kuwa wanawajibika kwa vitendo vyao ikiwemo pia uamuzi wanaochukua kwa niaba ya wananchi wa Bangladesh.
Ili kuhakikisha kila mtoto na mkazi wa Bangladesha anapata fursa sawa, Bwana Yunus amesema wanapatia kipaumbele huduma za elimu bora na afya bora, hatua ambazo zitawezesha kila mtu kustawi kwa kadri ya uwezo wake.
Apongeza vijana wa sasa ‘Gen Z’
Mshauri huyu Mkuu wa serikali ya mpito ya Bangladesh ametumia hotuba yake kuzungumzia vuguvugu lililoanzishwa na vijana wa kizazi cha Z au GenZ akiwafananisha na Mapinduzi ya Pepo za Monsuni.
“Tunaamini mapinduzi ya monsuni ambayo dunia imeshuhudia nchini Bangladesh kwa wiki kadhaa, yanaweza kuhamasisha jamii na dunia nzima kusimama kidete kutetea uhuru na haki,” amesema Bwana Yunus huku akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kushirikiana na Bangladesh mpya inayolenga kusaka uhuru, demokrasia kivitendo na kwa kila mtu.
Serikali ya mpito ilianzishwa Bangladesh na Bwana Yunus kuchaguliwa kuwa Mshauri Mkuu baada ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina kujiuzulu na kukimbia nchi tarehe 5 Agosti 2024 kufuatia maandamano makubwa dhidi ya serikali, maandamano yaliyosababisha vifo vya mamia ya waandamanaji.
Ghasia zilianza mwezi Julai mwaka huu kwa maandamano ya wanafunzi dhidi ya uwiano wa ajira za serikali. Ingawa mfumo huo ulifutwa, maandamano yaliibuka tena wiki iliyopita kwa ombi mahususi la kumataka Waziri Mkuu Sheikh Hasina aachie madaraka, na wahusika wa kukandamiza maandamano wawajibishwe.
Bwana Yunus amesema tayari wamefungua mchakato wa uchunguzi wa watu wote waliotoweshwa wakati wa utawala uliopita nchini humo.