Nenda kwa yaliyomo

Hawaa (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyota za kundinyota Hawaa (Ophiuchus) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Hawaa - Ophiuchus jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini

Hawaa (kwa Kilatini na Kiingereza Ophiuchus) [1] ni jina la kundinyota kwenye angakaskazi ya Dunia yetu.

Mahali pake

Hawaa - Ophiuchus lipo kwenye ikweta ya anga likionekana karibu na kanda ya Njia Nyeupe.

Linapakana na makundinyota jirani ya Hayya (mkia) (Serpens), Ukabu (Aquila), Rakisi (Hercules), tena Hayya (kichwa) , Mizani (Libra), Akarabu (Scorpius) na Kausi (Mshale) (Sagittarius).

Kundinyota la Hayya linakatwa na Hawaa. Hii inalingana na mitholojia ya Kigiriki ambako Hawaa ni mhusika anayebeba au kushindana na nyota inayoonekana kwa pande zake zote mbili.

Jina

Hawaa (Ophiuchus) lilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu wanaosema حواء ḥawwaaʾ wakimtaja mtu anayechezea nyoka [2]. Waarabu walifuata hapa mapokeo ya Wagiriki wa Kale waliosema Ὀφιοῦχος ofiukhos yaani “mwenye nyoka”; Ptolemaio aliingiza kundinyota kwa jina hili katika orodha yake ya Almagesti[3].

Wagiriki wa Kale waliona Ophiuchus - Hawaa kama nusu mungu Askulapius aliyeabudiwa kama mganga mkuu[4]. Askulapius aliwahi kufundishwa matumizi ya madawa ya majani na nyoka na hivyo ishara yake ni fimbo linaloviringishwa na nyoka, ambalo hadi leo ni ishara inayotumiwa na maduka na makampuni ya madawa.

Ophiuchus - Hawaa ni kati ya makundinyota 48 yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika karne ya 2 BK. Iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa kimataifa wa astronomia [5] kwa jina la Ophiuchus. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Oph'.[6]

Nyota

Nyota angavu zaidi ni Alpha Ophiuchi au Rasalhague ("kichwa cha mwenye nyoka")[7]. Ina mwangaza unaoonekana wa mag 2.07 ikiwa umbali wa mwakanuru 47 na Dunia[8][9].

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miaka nuru)
Aina ya spektra
α 55 Rasalhague 2.08m 47 A5 III
η 35 Sabik 2.43m 84 A2.5 Va
ζ 13 Han 2.54m 458 O9.5 V
δ 1 Yed Prior 2.73m 170 M1 III
β 60 Cebalrai 2.76m 82 K2 III
κ 27 3.19 m 86 K2 IIIvar
ε 2 Yed Posterior 3.23m 106 G8 III
θ 42 3.27m 563 B2 IV
ν 64 3.32m 153 K0 III
72 HR 6771 3.71m 83 A4 IVs
γ 62 3.75m 95 A0 V
λ 10 Marfik 3.8m 166 A2 V

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Ophiuchus" katika lugha ya Kilatini ni "Ophiuchi" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Ophiuchi, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. PAL - Glossary "Oph", tovuti ya mradi wa "Ptolemaeus Arabus et Latinus (PAL)" wa Bavarian Academy of Sciences and Humanities, iliangaliwa Oktoba 2017
  4. Allen uk 298: "the Serpent-holder generally was identified with "asklepios, Asclepios, or Aesculapius, .. with whose worship serpents were always associated as symbols of prudence, renovation, wisdom, and the power of discovering healing-herbs.”
  5. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  6. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  7. Tahajia "Rasalhague" inatokana na makosa wakati wa kunakili jina la "ras al-hawaa" kutoka mwandiko wa Kiarabu kwenda Kilatini.
  8. Ophiuchus], tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Oktoba 2017
  9. RASALHAGUE (Alpha Ophiuchi), tovuti ya Prof. Jim Kaler

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Argo Navis” ukurasa 374 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331