Wamasoni
Wamasoni (vilevile Masunia; kwa Kiingereza Freemasons yaani Waashi huru) ni chama cha siri kinachodai kufuata maadili na kustawisha udugu kati ya watu huru.
Msingi wake ni agano kati ya wanachama kwa ajili ya kushirikiana ili kufikia malengo ya pamoja.
Wamasoni wanatamka rasmi kutokuwa na ubaguzi wowote kati yao na kwa wanaotaka kujiunga nao, kufuatana na taratibu zilizopangwa katika Katiba ya waashi huru ambayo iliandikwa na James Anderson mwaka 1723 na inakubaliwa na miundo yote ya Kimasoni duniani ingawa kati yake kuna tofauti kadhaa kadiri ya mazingira.
Asili ya chama hicho haijulikani kwa hakika, hasa kabla ya mwaka 1650. Vilevile siri inayotawala maisha ya chama, hata kati ya ngazi mbalimbali za waliojiunga, inafanya iwe vigumu kuelewa malengo halisi na mbinu zinazotumika kuyafikia duniani kote.
Chama kinafanana na dini yenye madhehebu na ibada, hata kumbi zake zinaitwa mahekalu. Mungu anaitwa kwa kawaida Msanii majengo mkuu wa ulimwengu. Wakatoliki (na baadhi ya Wakristo wengine) hawaruhusiwi kujiunga na chama hicho.
Asili ya Wamasoni
Asili ya Wamasoni ilikuwa katika jumuiya ya waashi yaani mafundi waliojenga makanisa makubwa ya Ulaya wakati wa zama za kati. Wakati ule mafundi wa fani mbalimbali walipaswa kuwa wanachama wa jumuiya ya ufundi wao. Jumuiya hizo zilitunza elimu yao kama siri na wanachama walipaswa kuahidi kutunza siri za ufundi wao pamoja na siri za jumuiya. Wote walitakiwa kusaidiana.
Wakati wa kupokelewa, mwanachama mpya alitoa kiapo kilichofuatwa na viapo vingine baada ya kupanda ngazi katika ufundi wake.
Jumuiya hizo mara nyingi zilikuwa na salamu na maneno ya siri zilizosaidia kujtambulisha kama ndugu wa jumuiya wakati wa kufika katika mji mwingine.
Katika jamii ya Ulaya ya zama za kati jumuiya zote za mafundi zilikuwa pia na tabia ya kidini; kila mwanachama alipaswa kuwa Mkristo [1]; kwa kawaida kila jumuiya ilijiweka chini ya ulinzi wa mtakatifu fulani na kuanza mikutano yao kwa sala na ibada. Mfumo huu wa ufundi ulikwisha polepole.
Katika Uingereza jumuiya za waashi ziliendelea hata wakati ujenzi wa makanisa makubwa ulikuwa umepungua na elimu ya ufundi ilisambazwa zaidi tangu kuwepo wa uchapaji vitabu. Waashi walianza kupokea wanachama wasiokuwa wajenzi lakini waliendelea kujiita "Waashi huru".
Uhusiano kati ya jumuiya za waashi na Ukristo ulibadilika kutokana na matengenezo ya Kiprotestanti kwa sababu viongozi wa Kiprotestanti walijaribu kupiga marufuku jumuiya za mafundi zilizoendelea na ibada zenye tabia nyingi za Ukatoliki kati yao. Hata hivyo jumuiya za waashi ziliweza kuendelea kutokana na umuhimu wa ufundi wao. Maandamano kwenye siku za watakatifu yalizuiliwa.
Wakati wa zama za mwangaza fikra za falsafa mpya zilienea na jumuiya za waashi ziliwapa wanachama wao nafasi ya kujadili fikra hizo kwa uhuru zaidi kuliko jamii kwa jumla kwa sababu ya tabia ya kisiri ya mikutano yao. Hapo mawazo ya "dini ya kimantiki" yalitokea na kwa jumla waashi huru kati yao waliunda ibada zilizokazia maadili mema bila kutaja tena mafundisho ya Kikristo hasa. Wanachama walipaswa kukiri imani katika "roho mkuu" bila kutumia tena lugha ya kikristo au kukubali mafundisho ya Kanisa. Walilenga kuunganisha Wakristo wa madhehebu mbalimbali pamoja na Wayahudi na watu waliokataa imani ya dini yoyote.
Kutoka Uingereza Wamasoni walienea hadi Ulaya bara na pia Marekani, baadaye pia katika makoloni mbalimbali.
Wanaendelea kutumia vyeo vya kale kwa wanachama. Mgeni anapokewa kama mwanagenzi (apprentice), anaendelea kuwa fundi (fellow) na mwenyekiti au msimamzi wa jumuiya ya kieneo huitwa gunge (master). Jumuiya zao za kimahali zinaitwa nyumba (lodge).
Tanbihi
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |