Ibn Khaldun
Ibn Khaldūn (jina kamili kwa Kiarabu ni أبو زيد عبد الرحمن بن محمد بن خلدون الحضرمي Abū Zayd ‘Abdu r-Raḥman bin Muḥammad bin Khaldūn Al-Hadrami; mara nyingi kama Abdul Rahman Ibn Khaldun) alikuwa mtaalamu Mislamu kutoka Afrika ya Kaskazini alyieishi wakati wa karne ya 14. Alizaliwa mjini Tunis mnamo 1332 akaishi baadaye Fez na Granada na miaka ya mwisho alikaa Kairo alipokufa 1406.
Kimaitaifa anajulikana hasa kam mtaalamu bora wa historia. Lakini anatazamiwa pia kama mtangulizi muhimu katika fani kama falaki, uchumi, fiq-hi, hisabati, elimu ya jamii.
Taarifa juu ya maisha yake
[hariri | hariri chanzo]Aliandika mwenyewe kitabu cha "at-ta'rif bi-Ibn Chaldun wa-rihlatuhu gharban wa-scharqan / التعريف بابن خلدون ورحلته غربا وشرقا / taarifa ya Ibn Khaldun juu ya safari zake za magharibi na mashariki". Hasemi mengi juu ya maisha yake ya binafsi lakini anajieleza aliposoma, walimu wake na vitabu alivyosoma. Alikuwa mtoto wa familia ya makabaila walioitwa "banū chaldūn" walioishi miaka mingi huko Andalusia (Hispania ya Kiarabu). Kiasili walitoka katika Yemeni. Wakati wa rekonkista yaani kipindi ambako Wahispania wenyewe walianza kuwasukuma Waarabu kutoa maeneo mengi ya nchi yao akina banu khaldun walihamia Afrika ya Kaskazini. Hapa mababu kadhaa wa Ibn Khaldun walipata vyeo muhimu chini ya watawala Waislamu. Babu na baba yake waliacha siasa wakajiunga na tarikat ya Wasufi.
Masomo na maisha
[hariri | hariri chanzo]Kijana Ibn Khaldun alisomeshwa na walimu bora wa Afrika ya Kaskazini akasoma qurani, lugha ya Kiarabu, ahadith, fiq-hi, hisabati, mantiki na falsafa. Hapa alisoma hasa kazi za Ibn Rushd (Averroes), Ibn Sina Avicenna, Razi na at-Tusi. Alipokuwa na miaka 17 wazazi walikufa kutokana na ugonjwa wa tauni.
Alifuata mapokeo ya familia akitafuta ajira serikalini kwa watawala malimbali wa Afrika ya Kaskazini. Nia hii ilimpeleka katika maisha ya hatari yingi kwa sababu wakati wake watawala walibadilika haraka wakiangushana na kuwa na vita kati yao. Kwa hiyo Ibn Khaldun alipata vvyeo vikuu vilivyofuatwa na vipindi katika jela na miaka alipopaswa kukimbia nchi yake.
Tunis, Granada na Afrika ya Kaskazini
[hariri | hariri chanzo]Ajira ya kwanza ilikuwa kwenye ikulu ya mtawala wa Tunis alipokuwa na miaka 20. Alipewa cheo cha kātib al-ʿalāma كاتب العلامة yaani karani na mwandishi aliyetoa amri na matangazo rasmi ya sultani kwa maandishi mazuri. 1357 alitupwa jela kwa miezi 22 hadi sultani alikufa na mfuasi wake alimrudishia cheo chake. Alipanda ngazi hadi kuwa katibu mkuu wa mtawala. Sultani huyu alipopinduliwa aliondoka Tunis akaenda Granada ya Andalusia alipopokelewa vema na amiri Muhammad V aliyemfanya balozi wake kwa mfalme Mkristo wa Kastilia Pedro I akafaulu kupatana na mfalme a kupata mkataba wa mani kati ya Kastilia na Granada. Baada ya kurudi Granada alionewa mafanikio yake na waziri wa amiri akapaswa kuondoka tena akarudu Afrika ya Kaskazini.
Hapa alitumikia watawala mbalimbali wa madola madogo ya Kiislamu katika eneo la Algeria ya leo. Baada ya kuchoka siasa akaenda kuishi katika eneo la Waberber waliojitegemea akaanza kuandika kitabu cha historia ya dunia kati ya 1374–1377. Lakini hapa porini alikosa vitabu vya marejeo alivyohitaji kwa kazi yake akahamia tena Tunis.
Sultani mpya wa Tunis alimwajiri lakini Ibn Khaldun alikuwa na wasiwasi juu ya siasa zake akaomba rukhsa ya kwenda hajj ya Maka kama mbinu wa kuondoka Tunis akapanda jahazi ya kwenda Aleksandria katika Misri.
Misri
[hariri | hariri chanzo]Misri ilikuwa dola tulivu iliyokuwa na kipindi cha tawala imara na maendeleo ya kiuchumi chini ya nasaba ya Mamaluki. Tena Aleksandria ilikuwa kitovu cha elimu na hapa aliendelea na masomo na utafiti wake. Lakini hata hapo alishindwa kukaa mbali na siasa kwa sababu mwaka 1384 sultani Barkuk alimteua kama profesa wa fiq-hi na qadi mkuu kwa dhehebu la maliki. Majaribio yake ya kuleta matengenezo katika fiq-hi jinsi Wamisri walivyozoe yaligonga ukuta aliona upinzani na kujiuzulu bada ya mwaka mmoja pekee.
Hapo aliamua kutekeleza nia ya awali akaenda kuhiji Maka. Baada ya kurudi kutoka Maka akaendelea kufundisha kwenye vyuo vya Aleksandria akarudishwa tena kama qadi kwa Wamaliki; alirudia kujiuzlu akarudishwa tena mara kadhaa kutokana na sifa zake za utaalamu katika cheo ambacho hakupenda.
Mwaka 1401 aliamriwa kushiriki katika vita ya sultani mpya al-Nasir Faraj dhidi ya Wamongolia chini ya Tamerlan huko Syria kama mshauri wa mtawala. Mjini Dameski Ibn Khaldun alijikuta akifungwa ndani ya mji ulioshambuliwa na jeshi la Tamerlan. Ibn Khaldun aliteuliwa na watu wa Dameski kwenda kama mbalozi wao mbele ya mtawala wa Wamongolia na kuomba radhi kwa mji. Hapa alikutana mara kadhaa na Tamerlan na kujadiliana naye juu ya mengi akaokoa mji mbele ya hasira yake.
1401 aliweza kurudi Misri alipoandika taarifa ndefu juu ya Wamongolia akaendelea kukamilisha vitabu vyake juu ya maisha yake mwenyewe na juu ya historia ya dunia.
Mwaka 1406 aliaga dunia mjini Alkesandria.
Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Ibn Khaldun kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |