Nenda kwa yaliyomo

Uhindi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Uhindini)
भारत गणराज्य
Bhārata Gaṇarājya

Jamhuri ya Uhindi
Bendera ya Uhindi Nembo ya Uhindi
Bendera Nembo
Kaulimbiu ya taifa: "Satyameva Jayate" (Kisanskrit)
Kidevanāgarī: सत्यमेव जयते
("Ukweli pekee hushinda")
Wimbo wa taifa: "Jana Gana Mana"
Lokeshen ya Uhindi
Mji mkuu New Delhi
28°34′ N 77°12′ E
Mji mkubwa nchini Mumbai
Lugha rasmi Kihindi, Kiingereza na lugha nyingine 21
Serikali Jamhuri ya Maungano
Ram Nath Kovind
Narendra Modi
Uhuru
-ndani ya Jumuiya ya madola
-kama Jamhuri
Kutoka Uingereza
15 Agosti 1947
26 Januari 1950
Eneo
 - Jumla
 - Maji (%)
 
3,287,590 km² (ya 7)
9.6
Idadi ya watu
 - 2018 kadirio
 - 2011 sensa
 - Msongamano wa watu
 
1,352,642,280 (ya 2)
1,210,193,422
384.8/km² (ya 31)
Fedha Rupia (Rs.)1 (INR)
Saa za eneo
 - Kiangazi (DST)
IST (UTC+5:30)
not observed (UTC+5:30)
Intaneti TLD .in
Kodi ya simu +91

-

1 Re. is singular


India katika mipaka yake iliyokubaliwa na wote, bila maeneo yanayogombaniwa na nchi tofauti.

Uhindi (pia: India) ni nchi kubwa ya bara la Asia, upande wa kusini, ikienea hasa katika rasi kubwa ya Bahari ya Hindi.

Kwa eneo ina nafasi ya saba duniani, lakini kwa idadi ya wakazi (1,352,642,280 mwaka 2018) ni nchi ya pili baada ya China. Kati ya nchi za kidemokrasia ndiyo yenye watu wengi zaidi duniani. Tena inakadiriwa kwamba miaka ya hivi karibuni itapiku China.

Imepakana na Pakistan, China, Nepal, Bhutan, Bangladesh na Myanmar.

Kiutawala Uhindi ni shirikisho la jamhuri lenye majimbo ya kujitawala 29 pamoja na maeneo ya shirikisho 7.

Mji mkuu ni New Delhi, lakini mji mkubwa zaidi ni Mumbai.

Historia

Historia ya awali

Binadamu walifika India kutoka Afrika kabla ya miaka 55,000 iliyopita. Uwepo wao wa muda mrefu, kwanza kama wawindaji-wakusanyaji waliozagaa barani, umefanya watu wa eneo hilo wawe na tofauti kubwa kati yao upande wa urithi wa kibiolojia, ambayo inapitwa na Waafrika tu.

Makazi ya kudumu yalianza magharibi, katika beseni la mto Indus, miaka 9,000 iliyopita, hata kuzaa ustaarabu maalumu (Indus Valley Civilisation) katika milenia ya 3 KK.

Kabla ya ukoloni

Kufikia mwaka 1200 KK, Kisanskrit cha Kale, mojawapo kati ya lugha za Kihindi-Kiulaya, kilikuwa kimeenea India kutoka Kaskazini-Magharibi, kikawa lugha ya Rigveda, mwanzoni mwa dini ya Uhindu. Hivyo lugha za Kidravidi zikakoma kaskazini.

Kufikia mwaka 400 KK, matabaka ya kudumu katika jamii yalikuwa yamejitokeza katika Uhindu. Hapo dini za Ubuddha na Ujaini zilitokea, zikipinga taratibu hizo za kibaguzi. Katika bonde la mto Gange yalianza madola ya Maurya na Gupta. Ndani yake hadhi ya wanawake ilirudi nyuma, na mtazamo wa kwamba baadhi ya watu hawatakiwi hata kuguswa ukaimarika. Huko India Kusini, Falme za Kati zilieneza maandishi na tamaduni vya lugha za Kidravidi kwa falme za Asia Kusini Mashariki.

Kati karne za kwanza baada ya Kristo, dini za Ukristo, Uislamu, Uyahudi na Uzoroastro pia zilitia mizizi katika pwani za Kusini.

Majeshi kutoka Asia ya Kati yalivamia kwa kwikwi mabonde ya India, hata kuunda usultani wa Delhi na kuingiza India Kaskazini katika umma wa Kiislamu.

Katika karne ya 15 BK, Dola la Vijayanagara liliunda utamaduni wa kudumu wa Kihindu kusini mwa India. Katika Punjab, Usikh ulianzishwa, ukipinga dini rasmi.

Dola la Mughal, mwaka 1526, liliwezesha karne mbili za amani na kuacha urithi wa usanifu majengo bora.

Wakati wa ukoloni

Vituo vya nchi za Ulaya huko Uhindi miaka 1501-1937

Uhindi wa Kiingereza ni kipindi cha historia ambapo nchi za Bara Hindi ama zilitawaliwa na Uingereza moja kwa moja ama zilikuwa chini ya usimamizi wa Uingereza kama nchi lindwa.

Utawala huo ulienea juu ya Uhindi wa leo pamoja na Pakistan, Bangladesh, Nepal na kwa muda pia juu ya Burma (Myanmar).

Utawala wa Kiingereza ulikuwa na vipindi viwili vifuatavyo:

Utawala wa Kampuni ya Kiingereza kwa Uhindi wa Mashariki (British East India Company)

Tarehe 31 Desemba 1600 malkia Elizabeth I alitoa hati ya ulinzi wa kifalme kwa biashara kati ya Uingereza na "Uhindi wa Mashariki".

Kampuni iliyopokea hati hii ilikuwa kundi la wafanyabiashara na matajiri wa London waliovutwa na utajiri wa nchi za mashariki na hasa na faida kubwa mikononi mwa wafanyabiashara Wareno na Waholanzi waliotangulia katika biashara kati ya Ulaya na nchi za Asia ya Kusini.

Kampuni ilishindana kibiashara na kivita na wafanyabiashara wa Ureno, wa Uholanzi na wa Ufaransa. Iliweza kununua au kuvamia vituo vya biashara na kujenga maboma yake kuanzia mwaka 1644 huko Bombay, Madras na penginepo.

Mwaka 1717 kampuni ilipata kibali cha mtawala wa Moghul cha kusamehewa kodi kwa biashara katika Ubengali.

Tangu mwaka 1680 kampuni ilianzisha jeshi lake la maaskari Wahindi na kuwa mshiriki katika siasa ya Uhindi.

Kati ya miaka 1756 na 1763 Uingereza pamoja na mataifa mengine ya Ulaya ilishiriki katika Vita vya miaka saba viliyokuwa vita vya kwanza vya kimabara. Waingereza walipigana pamoja na Prussia dhidi ya Austria, Ufaransa, Urusi na Uswidi. Jeshi la kampuni liliendesha vita hivyo dhidi ya maeneo ya Ufaransa katika Uhindi. Wafaransa walishindwa wakabaki na vituo vidogo tu katika miji kama Pondicherry na Mahe lakini kampuni iliongeza maeneo yake katika Uhindi.

Baada ya mwaka 1757 Kampuni ya Kiingereza ilikuwa enzi muhimu, iliweza kushindana hata na nguvu ya Moghul. Ilianza kutawala sehemu kubwa za Uhindi wa Kusini pamoja na Ubengali.

Kampuni ilitumia mbinu mbili:

  • mikataba na madola ya watawala wa Kihindi waliokubali kupokea mabalozi wa kampuni kwao waliokuwa kama washauri wakuu wa Maharaja au Nawab wa eneo; siasa ya nje na mambo ya jeshi ziliwekwa chini ya kampuni
  • uvamizi na utawala wa moja kwa moja, maeneo yale yalikuwa mali ya kampuni.

Mafaniko makubwa ya kampuni yalisababisha mgogoro huko Uingereza na sheria mbalimbali za bunge la Uingereza zililenga kuongeza athira ya serikali ya Uingereza juu ya shughuli za kampuni.

Katika karne ya 19 kampuni ikawa mtawala wa sehemu kubwa za Uhindi, ama kwa njia ya mikataba na watawala wa kienyeji au kwa utawala wa moja kwa moja. Kampuni ilianza kubadilisha uso wa India kujenga reli na kuanzisha mawasiliano wa kisiasa kwa huduma ya posta na pia simu za telegrafi.

Mwaka 1857 ilitokea uasi wa wanajeshi Wahindi wa jeshi la kampuni uliosababisha na mkasi wa mabadiliko na dharau ya viongozi Waingereza kwa utamaduni wa wenyeji. Utawala wa kampuni ulianza kuporomoka; uliokolewa tu kwa kupeleka Uhindi wanajeshi kutoka Uingereza. Uasi ulikomeshwa kwa mabavu.

Lakini kuingilia kati kwa serikali ya Uingereza kulikuwa mwisho wa utawala wa kampuni. Mwaka 1858 serikali ya London ilichukua madaraka yote ya kampuni ikafanya Uhindi kuwa koloni la taji la Uingereza.

Uhindi wa Kusini au Jimbo la Madras mnamo 1909; nyekundu:koloni la Uingereza; njano: madola ya watawala Wahindi chini ya Uingereza (nchi lindwa)

Utawala wa kiserikali kati ya 1858 hadi 1947

Kuanzia mwaka 1858 Uhindi ulitawaliwa kama koloni la Uingereza. Kaisari wa mwisho wa Moghul Bahadur Shah Zafar II aliondolewa nchini. Malkia Viktoria wa Uingereza alichukua cheo chake akaitwa "Kaisari wa Uhindi" (kwa Kiingereza: "Empress of India"; kwa Kihindi: "Padishah-e-Hind") akamuachia utawala gavana wake aliyepewa cheo cha "makamu wa mfalme" (Vice-Roy).

Muundo wa utawala uliendelea: maeneo ya kampuni yalikuwa makoloni ya Uingereza. Maeneo ya watawala Wahindi yalibaki yalivyo lakini kila Maharaja au Nawab alipaswa kula kiapo cha utii kwa malkia kama Kaisari au malkia mkuu wa Uhindi na kumkubali mshauri Mwingereza katika jumba lake kama mwakilishi wa Uingereza.

Mwisho wa karne ya 19 harakati za kutafuta uhuru zilianza upya. Mwaka 1885 chama cha INC (Indian National Congress) kiliundwa na Wahindu na Waislamu pamoja waliodai uhuru. Mwaka 1906 viongozi Waislamu walitoka katika INC na kuunda "Shirikisho la Waislamu".

Mwaka 1917 Uingereza ulitamka ya kwamba ulitaka kuelekea polepole hali ya kujitawala kwa Wahindi. Viongozi wa wenyeji hawakuridhika na mkasi wa mabadiliko. Chini ya uongozi wa Mahatma Ghandi mwendo wa kupigania uhuru bila mabavu ulipata nguvu. Ghandi alipigania hasa umoja wa Wahindu na Waislamu lakini alipingwa na viongozi wenye itikadi kali wa pande zote mbili.

Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia Waingereza walikubali kujiondoa katika Uhindi. Swali kubwa lilikuwa kama nchi itabaki kama nchi moja au kama maeneo ya Waislamu yatajitenga.

Baada ya uhuru

Tarehe 14/15 Agosti 1947 utawala wa Uingereza ulikwisha. Bara Hindi iligawanywa katika nchi mbili za Uhindi na Pakistan. Mgawanyo ulikuja na vita na kumwaga kwa damu nyingi.

Tarehe 30 Januari 1948 Ghandi mwenyewe aliuawa na Hindu mkali aliyemchukia kwa sababu alitaka usawa wa Waislamu na Wahindu.

Mgawanyiko wa kiutawala

Hii ni orodha ya majimbo ya Uhindi:

Map of India showing its subdivision into states and territories.
Vijisehemu vya Uhindi, majimbo 28 na Union Territories 7.

Majimbo

  1. Andhra Pradesh
  2. Arunachal Pradesh
  3. Assam
  4. Bihar
  5. Chhattisgarh
  6. Goa
  7. Gujarat
  1. Haryana
  2. Himachal Pradesh
  3. Jammu na Kashmir
  4. Jharkhand
  5. Karnataka
  6. Kerala
  7. Madhya Pradesh
  1. Maharashtra
  2. Manipur
  3. Meghalaya
  4. Mizoram
  5. Nagaland
  6. Orissa
  7. Punjab
  1. Rajasthan
  2. Sikkim
  3. Tamil Nadu
  4. Telangana
  5. Tripura
  6. Uttar Pradesh
  7. Uttarakhand
  8. West Bengal

Maeneo ya Muungano:

  1. Visiwa vya Andaman na Nicobar
  2. Chandigarh
  3. Dadra na Nagar Haveli
  4. Daman na Diu
  5. Lakshadweep
  6. National Capital Territory of Delhi
  7. Puducherry


Watu

Mwanakijiji wa Kihindi katika mavazi ya jadi

Lugha ya taifa ni Kihindi, ambacho ni lugha ya Kihindi-Kiulaya, pamoja na Kiingereza ambacho pia ni lugha rasmi. Kuna lugha 21 kubwa na lugha nyingi zisizo na wasemaji wengi sana.

Kusini mwa Uhindi watu husema lugha za Kidravidi kama Kikannada, Kitelugu, Kitamil na Kimalayalam.

Kaskazini husema hasa Kipunjabi, Kibengali, Kigujarati na Kimarathi.

Lugha ndogo chache ambazo si lugha za Kihindi-Kiulaya (74 %) wala za Kidravidi (24 %) ni lugha za Kisino-Tibeti, lugha za Kiaustro-Asiatiki na lugha za Kitai-Kadai. Visiwani mwa Andaman, kulikuwa na lugha za Kiandamani lakini nyingi zao zimeshatoweka kabisa.

Wakazi walio wengi (79.8 %) hufuata dini ya Uhindu. Takriban 14.2 % ni Waislamu; hivyo Waislamu wa Uhindi ni jumuiya ya tatu katika umma wa Kiislamu duniani baada ya Waislamu wa Indonesia na Pakistan.

Dini nyingine ni Ukristo (2.3 %), Usikh (1,7 %), Ubuddha (0.7 %), Ujain (0.4 %), Uzoroastro na Bahai.

Tazama pia

Viungo vya nje

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Nchi na maeneo ya Asia

Afghanistan | Armenia2 | Azerbaijan | Bahrain | Bangladesh | Bhutan | Brunei | China | Falme za Kiarabu | Georgia2 | Hong Kong3 | Indonesia | Iraq | Israel | Jamhuri ya China (Taiwan) | Japani | Kamboja | Kazakhstan | Kirgizia | Korea Kaskazini | Korea Kusini | Kupro2 | Kuwait | Laos | Lebanoni | Macau3 | Malaysia | Maldivi | Mongolia | Myanmar | Nepal | Omani | Pakistan | Palestina | Qatar | Saudia | Singapuri | Sri Lanka | Syria | Tajikistan | Timor ya Mashariki | Turkmenistan | Uajemi | Ufilipino | Uhindi | Urusi1 | Uthai | Uturuki1 | Uzbekistan | Vietnam | Yemen | Yordani

1. Nchi ina maeneo katika Asia na Ulaya. 2. Nchi iko Asia lakini inahesabiwa pia kati ya nchi za Ulaya kwa sababu za historia au utamaduni. 3. Eneo la pekee la China.


Makala hii kuhusu maeneo ya Uhindi bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Uhindi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.