Udongo
Udongo (pia: ardhi) ni sehemu ya juu kwenye uso wa nchi ambako mimea huweza kuota. Nao hutumiwa kwa kilimo.
Udongo wenyewe ni mchanganyiko wa vipande vidogo vya mwamba na madini yaliyosagwa pamoja na mata ogania kama mboji (mabaki ya mimea na wanyama yaliyooza) na pia wadudu na vijidudu vinavyoishi ndani yake. Udongo huwa pia na hewa na maji ndani yake zinazojaza nafasi kati ya vipande vidogo vya mwamba.
Kiasi chake kikubwa ni vipande vidogo vyenye asili ya mwamba au madini. Mwamba huvunjwa na maji, upepo na kutokana na athari ya joto / baridi kwa njia ya mmomonyoko. Hivi vipande vinaweza kuwa vidogo sana na kuonekana laini kama udongo wa ufinyanzi; au vigumu vyenye pembe kama punje za mchanga.
Udongo hupatikana kama tabaka juu ya mwamba unaofanya ganda la dunia. Mpaka wa chini wa udongo ni pale ambako mwamba mtupu unaanza; mpaka wa juu ni uso wa ardhi. Tabaka la udongo linaweza kuwa na unene wa kilomita kadhaa au sentimita chache tu.
Matabaka ya udongo
Udongo mzuri huwa ndani yake na matabaka A-B-C pamoja na tabaka ya mata ogania juu yake.
O) Mata Ogania: katika mchoro huu 2 sentimita za juu ambazo ni majani makavu na sehemu nyingine za mimea zilizokufa au kuanguka chini; hazikuoza bado kikamilifu lakini zinaendelea kuoza. Wadudu wengi wanaishi hapa wanaoendelea kuozesha mata hii.
A) Udongo wa juu: Tabaka ya udongo yenye kiasi kikubwa cha mada ogania ndani yake. Ndani yake kuna minyoo na vijidudu wengi wanaoendelea kula na kubadilisha mabaki ya majani yaliyomo mle kuwa madini au kampaundi ogania sahili zaidi. Kwa kazi yao wanasababisha kuwepo kwa mashimo na nafasi ndogo ndani ya udongo wa juu. Nafasi hizi zinasaidia kuingia na kutoka kwa gesi na kiowevu. Kutokana na uwingi wa viumbehai hivi vidogo udongo wa juu una uwezo wa kutunza maji ya mvua ndani ya nafasi zake. Hii yote ni muhimu kwa kustawi wa mimea inayotandiza hapa mizizi yao.
Kwa lugha nyingine kuwepo kwa viumbehai hivi vidogo ni muhimu kwa rutuba ya udongo. Uhaba wa mata ogania unasababisha pia uhaba wa viumbehai ndani ya udongo wa juu unaokosa rutuba jinsi ilivyo jangwani.
Katika tabaka la udongo wa juu maji ya mvua yanapita haraka zaidi na kwa hiyo madini yeyushi kama chuma, alumini, chumvi mbalimbali na mengine kutegemeana na uwingi wa mvua na hali ya udongo chini yake kiasi cha madini haya yanaweza kuwa haba zaidi.
B) Udongo wa chini: katika tabaka hii madini yaliyoyeyushwa katika udongo wa juu yanakusanyika. Hapo ni sababu ya kwamba kulima shamba kunaongeza rutuba maana kazi ya kuchimba inapelekea madini yaliyozama chini kwenda juu.
C) Mwamba mzazi: hii ni tabaka ya mwamba isiymegeka bado. Unaitwa mwamba "mzazi" kwa sababu vipande vidogo vya matabaka ya juu vya asili hapo; kwa hiyo mwamba mzazi una tabia nyingi za kikemia sawa na udongo wa juu.
Mizizi mirefu ya miti inaendelea kufika hadi sehemu ya juu ya mwamba mzazi na kutafuta hapa madini yeyushi yalizozama chini zaidi. Kwa njia hiyo inachangia mmomonyoko wa sehemu hii hata kama imefunikwa na udongo.
Marejeo
Tazama pia
Makala bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |